Na Mwandishi maalum.Pichani ni askofu wa kanisa Anglikana Dayosisi ya Ruvuma mhashamu Dk.Maternus Kapinga akitoa maoni yake kuhusu kufungwa kwa aliyekuwa kiongozi wa kuvuruga kanisa
MUASISI na kiongozi wa wakristo wa dhehebu la misa ya pili wilayani Mbinga mkoani Ruvuma Joseph Lombola amehukumiwa kifungo cha miezi 12 kwa kosa la kufanya vurugu katika kanisa la Anglikana la Kristo Mfalme mjini Mbinga.
Lombola ambaye pia ni katibu wa Tume ya Utumishi ya Walimu (TSD) wilayani Mbinga ametiwa hatiani pamoja na Martin Mawala aliyeachishwa upadre wa kanisa Anglikana kwa kutomtii Askofu wa Dayosisi ya Ruvuma.
Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Mbinga Frank Mahimbali akitoa hukumu alisema ameridhika na upande wa mashitaka kuwa washitakiwa bila uhalali walifanya vurugu wakati ibada ikiendeshwa na padre Andrew Nkomola wa kanisa la Kristo Mfalme mjini Mbinga.
Kutokana na hali hiyo ,mahakama iliwatia hatiani hivi karibuni na kuwahukumu kifungo cha nje cha miezi 12 kila mmoja na kwamba katika kipindi hicho hawatakiwi kufanya kosa la aina yoyote.
Awali mwendesha mashtaka wa polisi Inspekta Isaya alidai washitakiwa hao walitenda makosa hayo Agosti 16 ,2009 katika kanisa hilo ambapo washitakiwa waliingia kanisani na kwenda madhabahuni kisha waliondoa vitambaa,kutupa vitabu vitakatifu na sakramenti takatifu jambo ambalo lilisababisha vurugu kutoka kwa waumini.
Habari zaidi kutoka ndani ya kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma zinadai kuwa Lombola ambaye hivi sasa anatumikia kifungo cha mwaka mmoja ndiye kiongozi wa kikundi cha kidini kinachojiita Wakristo wa Misa ya Pili(SECT) ambacho kinaendesha shughuli zake mkoani Ruvuma bila uhalali wa kuwepo kisheria kwa kuwa hakina usajiri wowote.
Askofu wa kanisa Anglikana Dayosisi ya Ruvuma Dk.Maternus Kapinga amesema amani ya kanisa hilo itaimarika zaidi baada ya kufungwa kwa muasisi wa SECT ambaye alikuwa ni muhimili wa kikundi cha Wakristo wa Misa ya Pili ambao kazi yao kubwa ni kulaghai,kuposha,kuharibu kanisa la Mungu na kuvuruga uongozi wa Askofu wa Ruvuma.
Kwa mujibu wa Askofu Kapinga waasisi,viongozi na wafadhili wakuu wa SECT ni wanasiasa,watu walioshindwa huduma takatifu na watu wanaowania vyeo na mali katika kanisa hilo ambao wamejiengua kutoka katika kanisa hilo kwa madai ya kutotaka kumtii Askofu wa Ruvuma wa awamu ya tatu.
“Lengo kuu la kikundi hicho ni kumwaga damu isiyo na hatia hasa wakidhamiria kumuondoa Askofu wa Ruvuma kutoka huduma takatifu aliyoitiwa na Mungu,mbinu kuu ambayo wanaitumia ili kutekeleza lengo hilo ni kupotosha na kutowaambia watu ukweli’’,alisema mkristo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini.
Mkristo huyo anabainisha zaidi kuwa kikundi hicho kinawashawishi watu wawafuate katika kumkataa Askofu wa Ruvuma na kwamba walifanikiwa kuanzisha vikundi katika maeneo ya Mbinga,Songea,Chiulu,Liuli na Puulu, vikundi ambavyo hivi sasa vyote vimekufa na wakristo wametubu na wamerudi kwa Askofu wa kanisa la Mungu.
Viongozi wa SECT ili kutimiza azima yao ya kulivuruga kanisa ,waliamua kuwaajiri makasisi waliosimamishwa ili wawe viongozi wao wa kiroho.Makasisi hao walisimamishwa kutoa huduma takatifu katika kanisa hilo baada ya kufanya makosa mabaya yakiwemo kuvunja ndoa, kutokutii mamlaka ya Mungu na kuishi na vimada.
Askofu Dk.Kapinga anasema waumini wa dhehebu la Misa ya Pili wamekuwa wakiigiza ibada zao kanisani na kwamba lengo lao halikuwa kumuabudu Mungu bali ni kuleta fujo ili ulimwengu useme Dayosisi ya Ruvuma ni yenye ni migogoro.
“Watu waliozuiwa kutoa huduma ya ukasisi katika kanisa hilo ,walikaidi amri hii ya Mungu na mamlaka halali ya kanisa,watu hao wakijua kuwa hawana mamlaka ya kasisi,lakini waliwadanganya watu na serikali kwa kuwaibia malipo,mathalani kwa kufungisha ndoa bila kulipia kibali cha kufungisha ndoa’’,alifafanua Askofu Dk.Kapinga.
Kikundi cha cha dhehebu la Misa ya pili kilijitokeza hadharani Desemba mwaka 2007 na hadi mwaka 2010 kikundi hicho kilikuwa kimemalizika na Dayosisi ya Ruvuma kuwa katika hali ya amani na utulivu kutokana na juhudi zilizozaa matunda kwa ushirikiano baina ya waumini,uongozi wa kanisa na viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali mkoani Ruvuma.
Takwimu toka ofisi ya Askofu wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Ruvuma zinaonesha kuwa hadi kufikia Oktoba 31 mwaka huu kanisa hilo lina jumla ya waumini 41,000 ambapo dhehebu la Misa ya Pili lina waumini wasiozidi 50(hamsini).
Makala hii kwa hisani ya kanisa Anglikana Dayosisi ya Ruvuma